Wabobezi katika
sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi wamekutana nchini Tanzania
katika kongamano kwa ajili ya kujadili mchango wa kukabiliana masuala
mbalimbali ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Kongamano hilo
limeratibiwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Chuo
Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela, likijumuisha wataalamu wa
sayansi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tasnia zinazohusiana kutoka Tanzania
na Afrika Mashariki.
Akifungua
kongamano hilo Mwenyekiti wa Bodi ya TMA Jaji Mshibe Ali Bakari,
amesisitiza ushiriki wa wataalamu wengi kutoka Afrika Mashariki katika mchakato
wa IPCC kutoka Afrika Mashariki.
“Ni matumaini
yangu kuwa kupitia makongamano kama haya ya uhamasishaji wa wanasayansi
kujihusisha katika kufanya tafiti zinazokidhi matakwa ya IPCC, wataalam wengi
zaidi kutoka Afrika Mashariki wataweza kutoa mchango kikamilifu katika
utayarishaji wa ripoti za tathmini ya Saba ya mabadiliko ya hali ya hewa na
tabianchi ya IPCC (IPCC AR7)” amesema Jaji. Mshibe
Naye, Kaimu
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa
IPCC, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema kuwa ripoti za IPCC zimekuwa na mchango
mkubwa katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi
kimataifa na nchi moja moja.
Dkt. Chang’a
amesema kuwa ripoti ya IPCC ya AR7 inayoandaliwa inatarajiwa itakuwa na jukumu
muhimu katika mustakabali wa hatua za kuchukua dhidi ya mabadiliko ya hali ya
hewa natabianchi kwa kuzingatia taarifa za kisayansi.
“Taarifa hizo
zitakuwa zimehakikiwa vyema ambapo zina mchango mkubwa katika kuongeza
ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi kikanda na
Duniani kote,” amesema Dkt. Chang’a.
Kongamano hilo
limeandaliwa mahsusi kwa ajili ya kuongeza uelewa kuhusu shughuli za Jopo la
Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Ripoti
zitakazoandaliwa katika mzunguko wa saba wa IPCC (AR7) kuhusu tathmini ya
mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na fursa za kushiriki katika mchakato
huo.
Mchakato huo
ikijumuisha uandishi, uteuzi wa wataalamu na mapitio ya ripoti za IPCC pamoja
na kuhamasisha wanasayansi hasa vijana, watendaji, wakufunzi na wanafunzi
kufuatilia na kushiriki katika mchakato mzima wa shughuli za IPCC katika
mzunguko wa saba ulioanza mwaka 2023 na unatarajiwa kumalizika mwaka 2029 au
2030.
0 Comments