Header Ads Widget

Responsive Advertisement

Uongozi wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi kuwapatia mafunzo wafanyakazi.


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema wakati umefika kwa Uongozi wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi kuwapatia mafunzo wafanyakazi yatakayo wajengea uelewa wa kuzifahamu vizuri sheria za utumishi, haki, wajibu pamoja na kujua stahiki zao.


Ameyasema hayo wakati akizungumza na Uongozi wa ZATUC uliofika Ofisini kwake Vuga kwa lengo la kujadili mambo mbali mbali yahusuyo Serikali na Vyama vya wafanya kazi.


Amesema umakini, usimamizi na utatuzi wa changamoto za wafanyakazi kwa Taasisi husika unahitajika ili kupunguza msururu wa malalamiko ambayo mengi yao yanakuwa tayari yameshasikilizwa na kupatiwa ufumbuzi.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema kwa kiasi kikubwa Serikali imekuwa ikilipa kipaombele suala la stahiki zote muhimu za wafanyakazi kwa kusimamia, kufanya marekebisho na maboresho ya maslahi ya wafanyakazi wa Umma kama sheria za Utumishi Serikalini zinavyoelekeza.


Mhe. Hemed amevitaka vyama vya wafanyakazi kuwakumbusha wanachama wao suala la haki na wajibu wa mfanyakazi jambo ambalo litasaidia kuondokana na tabia ya kufanya kazi kwa mazowea na kutoa msukumko kwa kila mfanyakazi kuwajibika kwa nafasi yake kwa kuzingatia taratibu za kazi na miongozo ya utumishi serikalini.


Aidha Mhe.Hemed ameahidi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuunga Mkono jihudi zinazofanywa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi na kuwa tayari kukutana nao ili kujadili mambo mbali mbali ikiwemo malalamiko yanayohitaji marekebisho ya sheria katika utekelezaji wake ambayo yamekuwa yakichukua muda mrefu kupatiwa ufumbuzi kutokana na utatuzi wake unahitaji muda na umakini katika kufikia ufumbuzi wa malalamiko hayo.


Nae Katibu Mkuu wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi(ZATUC) ndugu Khamis Mwinyi Mohd ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuzifanyia kazi changamoto mbali mbali zinazowakabili wafanyakazi na kuzipatia ufumbuzi jambo ambalo linazidi kuongeza ari na hamasa kwa wafanyakazi kufanya kazi zao kwa bìdii na uweledi mkubwa.


Katibu Khamis amesema ZATUC inekuwa na changamoto ya kukosa uhuru wa kujiunga pamoja jambo linalowakosesha fursa ya kufanya kazi zao pamoja na ushirikishwaji katiaka ngazi za maamuzi.

Post a Comment

0 Comments