Watumishi wa Shirika la
Masoko ya Kariakoo wametakiwa kufanya mageuzi katika utendaji kazi kwa
kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo na taaluma walizonazo ili kufikia
malengo ya Taasisi na kuongeza tija.
Hayo yamesemwa na
Meneja Mkuu wa Shirika hilo, CPA Ashraph Yusuph Abdulkarim wakati alipozungumza
kwenye hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi iliyofanyika leo (Aprili 4,2025) Dar
es Salaam.
Meneja Mkuu huyo
alisema endapo watumishi watafanya kazi kwa nidhamu na uadilifu ni dhahiri
kwamba uzalishaji utaongezeka na mazingira ya kazi yataboreshwa na kuleta
ufanisi mzuri katika utendaji kazi wa Shirika.
“Nitashirikiana
na watumishi wenzangu kulifanya Shirika lisonge mbele na kujiendesha kwa tija
pamoja na kudhibiti uvujaji wa mapato, kuongeza vyanzo vya mapato na kuweka
mipango mizuri ya kibiashara” alisema CPA Ashraph.
CPA Ashraph amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa
kumuamini na kumteua kuongoza Shirika la Masoko ya Kariakoo kwa nafasi ya
Meneja Mkuu.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo Hawa Ghasia, pamoja na
kumkaribisha Meneja Mkuu huyo alimwagiza kusimamia kwa ukaribu mchakato wa
maandalizi ya ufunguzi wa soko la Kariakoo uliopangwa ukamilike mwezi huu
Aprili.
“Kazi yako kubwa kwa
sasa ni kuhakikisha soko la Kariakoo linafunguliwa mwezi huu Aprili ili
kuwezesha wafanyabiashara waweze kuingia ndani kuendelea na biashara kufuatia
mradi wa ujenzi na ukarabati wa soko kukamilika,” alisema Ghasia.
Ghasia alisisitiza kuwa
Bodi ya Wakurugenzi ina imani kubwa na Mtendaji Mkuu huyo kutokana na uzoefu
alioupata alipokuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili hivyo aweke mipango ya
kujenga masoko mengine maeneo ya Shirika ya Mbezi Beach na Tabata Bima.
Naye Mkurugenzi wa
Utawala na Rasilimaliwatu kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Emma Lyimo
aliyemwakilisha Katibu Mkuu kwenye hafla hiyo aliwasihi watumishi kutoa
ushirikiano kwa Meneja Mkuu huyo ili atimize majukumu yake kwa ufasaha na kusaidia
Shirika kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.
Mwisho
0 Comments