Na Mwandishi wetu
PWANI.
Serikali inatambua umuhimu wa kuwawezesha watu wenye mahitaji Maalum kushiriki katika shughuli za kiuchumi , hivyo kuna upendeleo maalum katika Ununuzi wa Umma kwa ajili yao.
Hayo yamesemwa leo tarehe 25 Aprili, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma Bw. Dennis Simba wakati akifungua mafunzo kwa watu wenye mahitaji maalum katika Ununuzi wa Umma.
Amesema mafunzo haya yamekusudia kuelimisha na kuhamasisha makundi maalum juu ya haki zao na fursa wanazoweza kuzitumia katika mchakato wa Ununuzi wa Umma hivyo tunataka kuona makundi haya yanapata fursa za kibiashara ili kuchangia ukuaji wa uchumi wa Nchi.
"mpaka sasa kuna jumla ya vikundi maalum 280 vilivyokamilisha usajili na uhuishaji wa taarifa zao katika Mfumo wa Ununuzi wa Umma (NeST) ambapo vikundi hivyo vimepata tuzo za mikataba zilizotolewa kwa makundi maalum ambazo jumla ni tuzo Mia Nne Arobaini zenye thamani ya Shilingi Bilioni 15 ambapo Vijana ni vikundi 163 sawa na 58% wanawake ni vikundi 96 sawa na 34% na wenye Mahitaji maalum (Walemavu) ni Vikundi 4 sawa na 2% na wazee Vikundi 17 sawa na 6% sasa kama unavyoona usajili ni mdogo na mahitaji ni kwamba kila kikundi kiwe na kati ya watu watono hadi 20 hivyo bado kunamuamko mdogo kwenye vikundi vya watu wenye mahitaji maalum na ndio maana PPRA tumeona kuna haja ya kukutana na viongozi wa TAB na TLB , Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ili tuweze kuimarisha jambo hili. Alisema Mkurugenzi Mkuu PPRA
Aidha Bw. Simba amesema, Mamlaka ya Ununuzi wa Umma inajukukumu la kuhakikisha kuwa Mifumo ya Ununuzi inazingatia usawa, haki na uwazi na kutoa mafunzo kwa watu mbalimbali na kuanzisha programu za uhamasishaji na kushirikiana na wadau muhimu ili kuhakikisha kuwa makundi haya maalum yanaelewa haki zao katika michakato ya Ununuzi wa Umma.
"Nataka kusisitiza kwamba kila mmoja wetu anajukumu la kuhakikisha kuwa anafaidika na fursa zinazotolewa kwa Makundi Maalum katika sekta ya ununuzi wa umma, Mafunzo haya ni mwanzo mzuri wa safari ya kuelewa na kutumia haki hizi katika kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza tija katika Uchumi wa nchi, hivyo nitumie fursa hii kuwashukuru kwa kujitolea na kujiunga na mafunzo haya na nimatumaini yangu kuwa mtachukua maarifa haya na kuyatumia katika shughuli zenu za kila siku" Alisistiza Mkurugenzi Dennis Simba
kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania Bw. Omary Itambu Amasi amewashukuru PPRA kwa kuwaletea mafunzo ambayo yatawasaidia katika kupata tenda mbalimbali ambazo wengine wasio na mahitaji maalum wanazipata.
" Hapo mwanzo tulishindwa kupata fursa za tenda kutokana na kukosa Elimu hii kwa hiyo leo PPRA mmekuja kutupa mkate au ufunguo ambao utafungua kila kitasa kwenye masuala ya ununuzi katika sekta za Umma hivyo niwapongeze sana lakini sana niwaombe huu sasa ni mzizi mliousimika na mzizi ukianza litakuja shina hatimae matawi maana yangu ni kwamba hiki kilichoanzishwa sasa ni jambo ambalo linahitajika katika maeneo yote 26 Tanzania Bara na niwaombe bajeti zenu zitukumbuke. Alisema Mwenyekiti Huyo.
Uendeshaji wa mafunzo hayo ni mwendelezo wa Mamlaka wa utoaji mafunzo kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma na Mfumo wa NeST ili kuwajengea uwezo wadau wote wa sekta hii nyeti nchini.
0 Comments