Osaka, Japan.
Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na hifadhi ya Mlima Kilimanjaro vimeonekana kuwa kivutio kikubwa katika maonesho ya uchumi na biashara maarufu EXPO Japan 2025 yanayoendelea katika jiji la Osaka Kansai Japan ambapo wageni kadhaa wamekuwa wakitaka kujua namna ya kuweza kufika na kujionea vivutio hivyo.
Katika banda la Tanzania kwenye maonesho hayo wageni hao wamekuwa wakipata maelezo kutoka kwa maofisa wa Tanzania na wengi wao kushangazwa na jinsi nchi hiyo ilivyokuwa na utalii wa vivutio vingi vya kuvutia.
"Nimevutiwa sana leo kupata maelezo sahihi kuhusu hifadhi ya Ngorongoro,natamani siku moja kutembelea hifadhi hii ili niweze kuona wanyama hawa wanaoonekana kupitia picha mbalimbali, mimi ni mpenzi wa utalii wa kuangalia wanyama,alisema bi Matsuda Ikamoto mkazi wa Osaka.
Bi Ikamoto alisema kuwa kwa muda mrefu amekuwa akisikia kuhusu uwepo wa wanyama ambao hawafugwi katika maeneo ya kufugia wanyama na hivyo amepata maelezo sahihi kuhusiana na jinsi eneo la hifadhi ya Ngorongoro linavyoweza kuwalinda na kuwatunza wanyama hao.
Naye Bw. Yuri Toshiba alieleza matamanio yake ya siku moja kupanda mlima Kilimanjaro na hivyo kuweka historia kwa kuwa miongoni mwa wajapan waliopanda mlima huo.
Wengi wa watembeleaji wa maonesho hayo wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa Tanzania kuendelea kuvitunza vivutio hivyo ili viweze kuendelea kuwepo hasa kutokana na dunia kukumbwa na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi.
Akitoa maelezo kwa wageni mbalimbali waliotembelea maonesho hayo Afisa Utalii Mkuu kutoka Bodi ya Utalii Tanzania Bi Alistidia Karaze amesema Tanzania inaendelea kuimarisha vivutio na huduma kwa watalii ili kuongeza idadi ya watalii kila mwaka.
"Tanzania tuna vivutio vingi ambapo ukiachia utalii wa wanyama pia tuna fukwe mzuri pamoja na utalii wa malikale hivyo mtakapofika na kutembelea Tanzania mtafurahia vitu vingi ambavyo hamjawahi kuviona katika maeneo mengine.”alisema Bi Karaze.
Tangu kufunguliwa kwa maonesho hayo Tanzania imekuwa ikifanya vizuri kwa kupokea wageni wengi kwenye banda ambao wamekuwa wakielimishwa kuhusiana na masuala mbalimbali yanayohusu utalii,uchumi,biashara na sekta nyingine.