Header Ads Widget

Responsive Advertisement

MAKAMU WA RAIS ASHIRIKI IBADA YA SIKUKUU YA PASAKA


..................

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa wazazi hususani wakinamama kuwaongoza watoto wao hasa vijana kuacha tabia ya kushabikia vurugu wakati wa kampeni na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu.

Makamu wa Rais ametoa rai hiyo mara baada ya kushiriki Ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege Dodoma. Amewasihi Watanzania kushiriki Uchaguzi Mkuu kwa amani na utulivu kwa kuwa vurugu sio sehemu ya jadi ya Watanzania.

Aidha Makamu wa Rais ametoa wito kwa wote watakaopata dhamana ya kusimamia uchaguzi kuhakikisha wanazingatia sheria na miongozo watakayopewa pamoja na kutenda haki kwa wote watakaojitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi huo.

Halikadhalika, Makamu wa Rais amewasihi watumiaji wa vyombo vya moto kuwa na busara na umakini katika matumizi ya vyombo hivyo ili kuepusha kupoteza Maisha ya watu barabarani.

Makamu wa Rais amewatakia heri na baraka watanzania wote katika kusherehekea Sikukuu ya Pasaka na kuwasihi kusherehekea kwa amani na furaha.

Ibada hiyo iliyohudhuriwa pia na Mwenza wa Makamu wa Rais Mama Mbonimpaye Mpango imeongozwa na Padre Dionis Paskal Safari. 

Post a Comment

0 Comments