Mahakama ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza imemuhukumu Malimo Mathias Nguno kwa jina maarufu Gohe (41), kifungo cha miaka 30 jela baada ya kumkuta na hatia ya kumbaka mtoto (13) mwenye ulemavu wa kusikia (kiziwi).
Hukumu hiyo imesomwa leo Aprili 08, 2025 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Ndeko Dastan Ndeko.
Kwa mujibu wa hakimu Ndeko, mshtakiwa alitenda kosa hilo katika kesi hiyo ya jinai namba 2904/2025 kinyume na vifungu namba 130(1)(2)(e) na 131(1) vya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.
“Baada ya kupitia vifungu vya sheria na kujiridhisha na ushahidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri ambao haukuaacha shaka lolote na hivyo mahakama hii imekukuta na hatia ya kumbaka kigori (13) ) (jina limehifadhiwa),” amesema Hakimu huyo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshatakiwa alitenda kosa hilo mnamo tarehe 04.01.2025, katika Kijiji cha Nyambuyi kilichopo ndani ya wilaya ya Kwimba mkoa wa Mwanza kwa mwathiriwa ambaye ana ulemavu wa kusikia na kuongea maarufu kama Kiziwi.
Aidha, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Juma Kipalo, amesema mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa alifikishwa kwa mara ya kwanza mbele ya Mahakama hiyo tarehe 04.02.2025 na kusomewa shtaka la kubaka ambapo mtuhumiwa alikana kutenda kosa hilo.
Upande wa mashtaka ulileta mashahidi watano akiwemo mhanga chini ya usaidizi wa kutafsiri lugha za alama na ishara toka kwa mwalimu na mtaalam wa lugha za ishara.
Aidha, mshtakiwa baada ya kusomewa hukumu hiyo alitakwa na mahakama hiyo kujitetea kwa nini asipewe adhabu kali, hali iliyopelekea mshatakiwa kuiomba Mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa umri wake ni mkubwa na kwamba kama atapewa adhabu kali ya miaka 30 atafia gerezani.
Hata hivyo, Hakimu Dastan Ndeko alitupilia mbali ombi hilo na kumhukumu kwenda jela miaka 30 ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia hizo.
0 Comments