Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, ameshiriki Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu za Afrika, uliojadili maeneo ya kipaumbele ambayo nchi za Afrika zinahitaji kuyasukuma kama agenda mahususi katika mikutano ya Kundi la nchi 20 Tajiri Duniani (G20) kwa mwaka 2025 ambapo Nchi ya Afrika Kusini ni mwenyekiti wa G20, Mkutano uliofanyika katika Ofisi za Kamisheni ya Umoja wa Afrika, kando ya mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Jijini Washington D.C, Marekani.
Aidha, majadiliano katika mkutano huo pamoja na mambo mengine, yaliangazia kuhusu Afrika kuwa na sauti moja katika kuzishawishi nchi za G20 kufanya mabadiliko yatakayosaidia upatikanaji wa fedha na mikopo nafuu kwa nchi zinazoendelea, namna ya kukabiliana na madeni, suala ambalo ni tatizo kwa nchi nyingi za Afrika kufuatia mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi, kijiografia na kisiasa.
Mkutano huo umehudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, Naibu Gavana wa BoT, Dkt. Yamungu Kayandabila, Mhasibu Mkuu wa Serikali, CPA Leonard Mkude, na Maafisa wengine waandamizi wa Serikali.