DCEA YAKAMATA KG.4,568 YA DAWA ZA KULEVYA,YAZUIA TANI 14 ZA KEMIKALI BASHIRIFU KUINGIA NCHINI

Kamishna Jenerali wa Mamlaka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo wakati akitoa taarifa kuhusu operesheni ya Mwezi machi hadi April mwaka huu ambayo wameifanya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola katika mikoa ya Dar es salaam,Shinyanga,Tabora,Songwe,Mbeya na Arusha.
Mkurugenzi Msaidizi Malalamiko kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU ) Thobias Ndaro akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam.

......................

 NA MUSSA KHALID

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata Kilogram 4,568 za dawa mbalimbali za kulevya na kuteketeza ekari 178 za mashamba ya bangi pamoja na kushikilia magari,pikipiki tano na bajaji moja vilivyohusika kwenye uhalifu huo.

Pia imefanikiwa kuzuia tani 14 za kemikali bashirifu zilizokuwa ziingizwe nchini kinyume na sheria pamoja na pakti 10 za pipi zenye uzito wa gramu 174.77

Hayo yameelezwa jijini Dar es salaam na Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo Aretas Lyimo wakati akitoa taarifa kuhusu operesheni ya Mwezi machi hadi April mwaka huu ambayo wameifanya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola katika mikoa ya Dar es salaam,Shinyanga,Tabora,Songwe,Mbeya na Arusha.

Kamishna Lyimo amesema kuwa katika operesheni zilizofanyika mkoani Mbeya,raia wa Uganda Herbert Kawalya mwenye hati ya kusafiria Na.B00132399  na mmiliki wa Kampuni ya Hoxx Wells Lux Tour Limo alikamatwa akiwa na pakti 10 za pipi zenye uzito wa gramu 174.77 zilizotengenezwa kwa dawa aina ya bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu ya tetrahydrocannabinol (THC).

“Aidha katika tukio lingine Mkoani Mbeya zilikamatwa kilogram 1658 za bangi aina ya skanka na kilogram 128.7 za bangi zilizokuwa zinaingizwa nchini kutoka Malawi’amesema Kamishna Lyimo

Ameendelea kusema kuwa katika operesheni waliyoifanya jijini Dar es salaam,zilifanikisha ukamataji wa kilogram 220.67 za bangi aina ya skanka katika kata yaChanika zikiwa zimefichwa chooni huku kilogram 11 zikikamatwa eneo la ukaguzi wa mizigo kwenye bandari ya kuelekea Zanzibar

“Katika operesheni zilizofanyika mikoa ya Arusha,Tanga na Manyara zilikamatwa Kilogram 733.74 za dawa za kulenya aina ya Methamphetamine,kilogram 91.61 za heroin,kilogram 692.84 za mirungi iliyokuwa inaingizwa kutokea nchini Kenya na Kilogram 115.05 za bangi pamoja na kuteketeza ekari mbili za mashamba ya bangi’amesema Kamishna Lyimo

Vilevile Kamisha Lyimo amesema katika operesheni zilizofanyika Wilaya ya Uyui na Nzega mkoani Tabora,Kilogram 845 za bangi zilikamatwa na ekari za mashamba ya bangi ziliteketezwa.

Katika hatua nyingie Kamishna Jenerali Lyimo ametoa wito kwa watendaji wa serikali za mitaa kudhibiti uhalifu huo katika maeneo yao na watachukuliwa hatua endapo watashindwa kukomesha na wakibainika kuhusika katika uhalifu huo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Malalamiko kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU ) Thobias Ndaro amesema watahakikisha wanafuatilia kwa umakini watumishi wa umma ambao wanachangia au kuenea kwa changamoto ya dawa za kulenya nchini.

Ametumia fursa hiyo kutoa wito wa watumishi wa umma kuwa waadilifu kwa kutochangia madawa ya kulevya kushamiri katika maeneo yao.

Hata hivyo wazazi na walezi mnahimizwa kuwa makini na kufuatilia kwa karibu mienendo ya watoto wenu ikiwa ni pamoja na kuwaasa wajiepushe na mazingira na sababu zozote zinazoweza kuwaingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya.


mussa khalidi

I am ,Journalist, Presenter Radio & TV, Producer, Video editor, Graphics Designer, Layout Newspaper designer,Contact: +255 659 669 902 Email: mussakhalid70@yahoo.com or muxabhai200@gmail.com

Post a Comment

Previous Post Next Post