



(Picha na Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini WF, Mwanza)
Na. Josephine Majura, WF, Mwanza
Watumishi wa Umma na Sekta Binafsi wameshauriwa kujifunza kuhusu uwekezaji mapema ili kuhakikisha kuwa baada ya kustaafu wanaendelea kuishi maisha mazuri, kama walivyokuwa kazini.
Ushauri huo umetolewa na Afisa Masoko Mwandamizi, Kampuni ya Uwekezaji ya UTT – AMIS, Bw. Rahim Mwanga, wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa kwa watumishi wa Halmashauri hiyo na Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Taasisi zake.
Aliongeza kuwa kustaafu hakupaswi kuwa chanzo cha matatizo ya kifedha, kwa mfanyakazi yoyote aliyekuwa analipwa mshahara bali iwe fursa ya kufurahia matunda ya kazi ya muda mrefu.
“Tukijijengea utamaduni wa kuwekeza mapema kutatusaidia sisi wafanyakazi kuepuka changamoto za kifedha baada ya kustaafu na kuwa na maisha ya uhakika”, alisema Bw. Mwanga.
Aidha aliwasisitiza wafanyakazi wote nchini kuhakikisha michango yao inalipwa kwa wakati na waajiri wao lakini pia watumie Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inayotoa faida kubwa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Bw. Erick Mvati, aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kufika katika Mkoa wa Mwanza kutoa elimu ya fedha ambayo ni muhimu kwa wananchi ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Aliongeza kuwa elimu hiyo ikifika kwa wananchi wote katika makundi mbalimbali itasaida kupunguza matatizo katika jamii kwa kuwa wananchi wataelewa haki zao lakini pia watajua sheria mbalimbali zitakazowaongoza na kujiepusha na migogoro ya mikopo.
Naye Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Santley Kibakaya, alisema kuwa Wizara inaendelea na zoezi la utoaji elimu ya fedha kwa wananchi ili wafahamu fursa mbalimbali zinazopatikana katika Sekta ya Fedha.
Aliongeza kuwa Sekta ya Fedha imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali, kupitia elimu hiyo inayoendelea kutolewa, wataalamu hao wanapata fursa ya kusikiliza changamoto, ushauri na maoni yanayotolewa na wananchi kwa ajili ya kufanyiwa utatuzi zile ambazo zinatakiwa kufanyiwa utatuzi, ushauri na maoni kwa ajili ya kuboresha zoezi hilo kwa mikoa ambayo haijafikiwa.
0 Comments