Header Ads Widget

Responsive Advertisement

PIC YATAKA WAKANDARASI KUMALIZA KWA WAKATI UJENZI KIWANJA CHA NDEGE MSALATO


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeuelekeza Wakala wa Barabara  Tanzania (TANROADS) kuhakikisha wanawasimamia Wakandarasi wanaotekeleza ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato ili kukamilisha ujenzi huo kwa wakati.


Maelekezo hayo yametolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo leo tarehe 12 Machi, 2025 jijini Dodoma na Mheshimiwa Augustine Vuma, mara baada ya Kamati hiyo kukagua na kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati ambapo Kamati imeshuhudia kazi kubwa iliyofanyika.


“Tunaipongeza Serikali kwa kuendeleza mradi huu, tumeona utekelezaji wake na kuridhika nao, upande wa jengo tunaona limefika asilimia 51  na linagharimu zaidi ya shilingi Bilioni  190 na barabara ya kuruka na kutua ndege imefika asilimia 85 ambayo inagharimu zaidi ya shilingi Bilioni 160, rai yetu ni kuwa mradi huu utakamilika kwa wakati kama ulivyopangwa”, amesema Mheshimiwa Vuma.


Mheshimiwa Vuma ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutachochea fursa za kiuchumi na kijamii katika mkoa wa Dodoma na nchi kwa ujumla kutokana na kuwepo kwa fursa nyingi za kibiashara na kiuwekezaji.


Aidha, Mhe. Vuma ameipongeza Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa usimamizi mzuri wa mradi huo na kuzingatia thamani ya fedha ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa ubora na kwa wakati.


Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi, Mohammed Besta  ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya mradi huo na ameahidi kuendelea kusimamia mradi huo ili kukamilika kwa muda uliopangwa.


Ameongeza kuwa mradi huo umetoa ajira nyingi kwa wazawa  kwani Wataalamu wengi walioshiriki katika ujenzi wa kiwanja hiki ni Watanzania, licha ya kuwa kampuni za ujenzi ni za Kichina.


Utekelezaji wa mradi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato unajumuisha ujenzi wa Jengo la Abiria, Jengo la kuongozea ndege, barabara ya kuruka na kutua ndege, eneo la maegesho ya ndege ambapo ujenzi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Julai, 2025 kwa mujibu wa mkataba.

Post a Comment

0 Comments