Header Ads Widget

Responsive Advertisement

ELIMU YA FEDHA KUYAFIKIA MAKUNDI YOTE


Serikali inatambua umuhimu wa kuhakikisha kwamba makundi yote maalumu, yakiwemo watu wenye ulemavu wa kusikia (viziwi), wanawake, vijana, na wazee, wanapata elimu ya fedha nchini ili waweze kujikwamua kiuchumi. 


Hayo yameelezwa na Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya , wakati wa mafunzo kwa watu wenye ulemavu wa kusikia yaliyofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Musoma mkoani Mara.


“Elimu hii inalenga kuyawezesha makundi haya kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, kuwajenga uwezo wa kusimamia rasilimali zao, na kuboresha maisha yao kwa ujumla”, alisema Bw. Kibakaya.


Alisema kuwa katika utoaji wa elimu ya fedha katika makundi mbalimbali nchini, washiriki wamepewa elimu katika maeneo ya usimamizi wa fedha binafsi, uwekaji  akiba, mikopo, uwekezaji, bima, bima ya amana, kodi na kujipanga kwa maisha ya uzeeni.


Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Bw. Athuman Khalid (mlemavu wakusikia) alieleza furaha yake kwa kupata fursa ya kushiriki mafunzo ya elimu ya fedha.


“Kwa muda mrefu tulihisi kutengwa katika masuala ya fedha, lakini leo tumefikiwa na kupewa elimu kuhusu kupanga matumizi, kujiwekea akiba, kufanya uwekezaji na kutumia Taasisi rasmi kuchukua mikopo”, alisema Bw. Khalid.


Naye Mkalimani, Bi. Dainess Wilson, aliiomba Serikali kuendelea kutoa mafunzo endelevu kwa Wakalimani nchini ili kuboresha ujuzi na weledi wao katika kazi na kutoa huduma za utaalamu wa hali ya juu na kuongeza tija katika utendaji wao.


Wizara ya Fedha kwa kutambua umuhimu wa mchango wa Taasisi za Fedha Timu ya Wataalamu kutoka wizarani ambayo ipo mkoani Mara kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali imeambatana na Wataalamu kutoka  Taasisi nyingine za Serikali, ikiwemo Kampuni ya Uwekezaji ya UTT AMIS na  NSSF, pamoja na Taasisi za Kibenki ikiwemo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Benki ya Biashara Tanzania (TCB), CRDB, NMB, NBC.

Post a Comment

0 Comments