Header Ads Widget

Responsive Advertisement

RC CHALAMILA AFUNGUA MKUTANO WA SIKU MBILI WA MAAFISA USTAWI WA JAMII-DSM


 Na Mwandishi wetu.

-Azindua vyombo vya Habari vya huduma za Ustawi wa Jamii.


-Asisitiza utoaji wa elimu kwa jamii juu ya maswala ya Ukatili wa kijinsia na kukemea vitendo hivyo.


Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Albert Chalamila Leo Agosti 6 2024 amefungua mkutano wa Maafisa Ustawi wa Jamii Mkoa katika Ukumbi wa Karimjee-Posta jijini Dar es Salaam ambao unatarajiwa kuhitimishwa Agosti 7 2024.


RC Chalamila akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano huo amesema, ni hatua kubwa  zilizofanywa na sekta hii ya Ustawi wa Jamii  kwakuwa dunia ya sasa mambo mengi yanayoendelea huonekana sana mtandaoni hivyo, vyombo hivi vya habari vitakuwa ni chanzo cha kufikisha taarifa na elimu kuhusu ustawi wa jamii kwa wakati husika. 


Aidha, Mheshimiwa  Mkuu wa Mkoa amezindua channel maalum ya mtandaoni ya ustawi wa jamii iitwayo "Ustawi wa Jamii Dsm Digital" na kukabidhi vifaa vya kuchakata habari ikiwemo computer mpakato(laptop), camera na vifaa vingine vitakavyotumiwa na vitengo vya ustawi wa jamii katika halmashauri za Manispaa zote za mkoa wa Dar es salaam.


Sanjari na hilo,RC Chalamila aliwataka Maafisa Ustawi wa Jamii kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa ili kuhakikisha huduma bora zinawafikia wananchi wote.Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano na rasilimali muhimu kwa maafisa hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.


Vilevile mkutano huu umetoa fursa ya kipekee kwa Maafisa Ustawi wa Jamii kubadilishana uzoefu, kujifunza na kuunda mtandao wa ushirikiano ambao utasaidia katika kuboresha huduma za kijamii nchini pamoja na kukemea vikali vitendo vya  ukatili wa kijinsia na taharuki za utekaji zisizo za kweli zinazoendelea kwenye jamii.


Mwisho RC Chalamila alikabidhiwa tuzo ya kutambua mchango wake katika ustawi wa jamii na kupata fursa ya kutoa tuzo kwa Katibu Tawala wa Mkoa Dkt. Toba Nguvila, Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt Mohammed Mang'una na viongozi wengine waliotangulia kwa kutambua mchango wao katika sekta hiyo.









Post a Comment

0 Comments