*Lengo ni kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati
*Aeleza umeme unavyochagiza shughuli za kiuchumi
*Vijiji 621 Morogoro vyafikiwa na umeme kati ya Vijiji 669
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Nishati kuongeza nguvu katika kusimamia miradi yote ya nishati ili ikamilike kwa wakati na hivyo kuwawezesha wananchi kupata nishati ya uhakika.
Rais Samia ametoa agizo hilo Agosti 06, 2024 wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.
"Nimejionea mwenyewe wakati naenda Kilosa tofauti iliyokuwa ikionekana maeneo ambayo hayana umeme na yale yenye umeme ambayo yameshamiri kwa shughuli za biashara, hii inaonesha umuhimu wa nishati katika maeneo yote nchini." Amesisitiza Dkt.Samia
Aidha, Rais Samia ameutaka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kukamilisha mapema kupeleka umeme kwenye Vijiji vilivyobaki na kuongeza kasi ya kusambaza umeme kwenye Vitongoji ili wananchi waweze kufanya kazi za maendeleo.
Aidha, amesisitiza kuwa uwepo wa umeme wa uhakika kutoka Bwawa la Julius Nyerere kunaufanya Mkoa wa Morogoro kuwa sehemu sahihi ya uwekezaji.
"Morogoro sasa ina umeme wa uhakika, hali inayovuta uwekezaji ndani ya Mkoa." Ameongeza Mhe.Rais
Akizungumzia kuhusu miradi ya umeme vijijini Mkoa wa Morogoro, Dkt. Samia amesema kupitia Wakala wa Nishati Vijijini Serikali imepeleka umeme kwenye Vijiji 621 kati ya Vijiji 669.
0 Comments