"Ndoto yangu kubwa ilikuwa kuwa mchezaji mpira lakini ilikwama kipindi ambacho wazazi hawakuelewa kuwa kuna haja ya kuendeleza vipaji,walikasirika kila nilipotoka shule na kiatu kimeharibika kwa sababu ya kucheza mpira wakati mimi ni binti, kwanini nicheze mpira’’
Loveness Stanley Tarimo 38 ,anasema anapenda kutambulika kama mwanamke wa kawaida kabisa anayejipenda na asiye na majivuno. Muonekano wake haumbadilishi jinsia yake na anajivunia kuwa alivyo.
Loveness amezaliwa katika familia ya watoto wa kike watatu na mmoja wa kiume huko mkoani Kilimanjaro.
‘’Mimi nimetokea kwenye familia ya kawaida ya kikristo kabisa ya wacha Mungu,ingawa mimi ninaonekana kama niko tofauti kidogo,’’anaeleza Loveness huku akicheka.
Nilipokuwa mtoto nilichukia kuitwa 'jike dume'
Baada ya kumaliza darasa la saba katika shule ya msingi Kijenge, Arusha Loveness hakubahatika kuendelea na masomo ya sekondari kwa kushindwa kupata ufaulu mzuri na wazazi hawakuwa na uwezo wa kumuendeleza katika shule za kulipia.
Hivyo aliamua kujikita zaidi kwenye michezo jambo alilofurahia sana katika kipindi chote.
Ingawa mazingira ya mpira wa miguu yakiwa ya chini sana kwa upande wake aliamua kuachana na mchezo huo kwani haukumlipa akaamua kujiunga na kujifunza mazoezi ya kujenga mwili.
‘’Maisha ya shule yalikuwa mazuri sana kwangu muda mwingi nilipenda kucheza mpira. Watoto wenzangu walinishangaa kwanini kila mara nilipokwenda uwanjani nilivaa sketi ya shule na kaptura kwa ndani ili nicheze mpira kwa uhuru’’anaeleza akitabasamu
Loveness anasema zipo nyakati hakufurahia wakati wa utoto wake akieleza namna baadhi ya wanafunzi walivyokuwa wakimtania kwa kumuita majina kama 'Tomboy' au jike dume kwa sababu tu alipenda kuongozana na wavulana, "Nilikuwa nikiitwa hivyo ninaenda chumbani ninalia".
‘’Hata nikihitaji kitu sasa hivi siwezi kuomba msichana,ni rahisi sana kumuomba mwanaume kuliko mwanamke."
Pamoja na kuwa tofauti kwa muonekano wa jamii, anajivunia kuwa hakuwahi kuwavunjia heshima wazazi wake, na wanajivunia kuwa na mtoto kama yeye.
Loveness anasema haikuwa rahisi kujenga mwili kuwa na misuli namna hii.
Ni takribani miaka 10 sasa tangu alipoanza kufanya mazoezi ya kujenga misuli,na sasa anafurahia muonekano wake kwani unampa utofauti na wanawake wengine,anajisikia mrembo zaidi.
Anasikitishwa na namna baadhi ya watu wasivyomtathmini na kumpa majina kama Tom boy na mtu ambaye amekataa jinsi yake, anasema inamshangaza haelewi tatizo nini.
‘’Kipindi cha nyuma kweli ilinisumbua lakini sasa hivi ninazidi kupenda nilivyo kwani hakuna kitu kizuri kama kujikubali.
Kwa maisha ya sasa hivi ukisema uhangaike na kila mtu ili akuelewe utasumbuka sana. Siwezi kuwalazimisha watu kunielewa nimeachana nao".
Muonekano wake umempa fursa ya kujiingizia kipato kwa kutoa mafunzo kwa watu mbalimbali ambao wamekuwa wakimfikia na kuwafundisha.
‘’Namshukuru Mungu nimekuwa nikipata sana wateja ambao wengi ni wanawake kidogo imeniongezea kipato’’
Idadi ya walimu wa mazoezi wa kike kuwa ndogo, kwa Loveness imekuwa fursa, "Wateja wangu wengi wa kuwafundisha mazoezi ni wanawake waislamu, wahindi na waarabu kwasababu ya imani yao wanaona ni bora wanichague mimi mwanamke kuliko kufundishwa na mwanaume. Wameshaniamini mimi ni jinsi ya kike na muonekano wangu hauwapi wasiwasi wowote, "Loveness anaeleza.
Loveness anasema ‘’Unajua wenzetu kidogo haiwasumbui kwani michezo hii ya wanawake kuwa na misuli mikubwa kwao ipo,lakini kwa hasa watanzania kushangaa nawaelewa tu’’
0 Comments