Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) Jenerali Venance Mabeyo (mstaafu) ameuelekeza uongozi wa mamlaka hiyo kuweka jitihada za kuboresha miundombinu katika kituo cha magofu ya Engaruka kilichosheheni historia ya teknolojia ya kilimo cha umwagiliaji kilichofanyika eneo hilo karne ya 14 hadi 18. Teknolojia hii inahusishwa na jamii ya wairaq na Wasonjo walioishi katika eneo la engaruka katika karne hizo.
Akiwa na wakurugenzi wa bodi ya NCAA, Jenerali Mabeyo ameeleza kuwa eneo hilo lililopo pembezoni mwa hifadhi ya Ngorongoro ni miongoni mwa vituo vya malikale vinavyosimamiwa na NCAA ambapo historia inaonyesha wakazi walioishi Engaruka karne ya 14 walitumia eneo hilo kwa shughuli za kilimo cha mazao mbalimbali yaliyostawi kutokana na uwepo wa maji ya kutosha yanayotiririka muda wote kutoka msitu wa nyanda za juu kaskazini katika hifadhi ya Ngorongoro.
“Simulizi kuhusu eneo hili zinahusisha shughuli zilizofanyika pamoja na jamii iliyoishi hapa, matokeo ya tafiti nyingi zilizofanyika katika eneo hili ipo makumbusho ya Taifa, lakini kwa kuwa NCAA tumekabidhiwa eneo hili tujipange kuboresha zaidi miundombinu ya barabara, choo cha kisasa, ofisi na maeneo ya kupumzikia wageni ili watalii waje kwa wingi kuona kivutio hiki na kujifunza teknolojia ya kilimo cha umwagiliaji ilivyokuwa, mazao yaliyokuwa yakilimwa, uhifadhi shirikishi kwa jamii inayozunguka hapa na kupata historia ya urithi wa utamaduni na zana zilizotumika katika kilimo” aliongeza Jenerali Mabeyo (mstaafu).
Mkuu wa kituo cha magofu ya Engaruka Bw. Jackson Tito ameueleza ujumbe wa wakurugenzi wa bodi kuwa, wageni wanaotembelea eneo hilo wanapata fursa ya kujua teknoloijia ya umwagiliaji kuanzia maandalizi ya mashamba, mifereji ya maji kwa ajili ya umwagiliaji, kuona masalia ya vyungu vya kupikia na mafiga yake na zana nyingine za kale zilizotumiwa na jamii iliyoishi katika eneo hilo.
Tito anaeleza kuwa baada ya NCAA kukabidhiwa eneo hilo imeanza kulifanyia maboresho kwa kufufua magofu yenyewe, kuanza ukarabati wa miundombinu, kufanya usafi wa eneo, kuweka vibao elekezi kwenye barabara kuu ya kutoka mto wa mbu kuelekea Loliondo, kuandaa vipeperushi vyenye taarifa ya eneo hilo na kuvisambaza kwa wadau, kuandaa ramani ya eneo kwa ajili ya wageni wanaotembelea sambamba na kushirikiana na jamii ya wamasai waliopo katika Kijiji cha Engaruka na wadau wa utalii ili kulitangaza zaidi eneo hilo na kupata wageni wa ndani na nje.
Kwa upande wake Afisa Uhifadhi mkuu na kaimu mkuu wa Idara ya Urithi wa Utamaduni na mambo kale Dkt. Agness Gidna ameeleza kuwa uongozi wa NCAA unaendelea kusimamia, kuhifadhi, kulinda, kuendeleza na kivipa thamani vituo vya malikale inavyovisimamia na kuviboresha ili kuongeza idadi ya wageni wanaopenda utalii wa mambo kale na urithi wa utamaduni.
Tangu mwaka 2019 Serikali ilikabidhi eneo la hifadhi ya Ngorongoro baadhi ya vituo vya malikale kwa ajili ya kuvihifadhi na kuviendeleza. Vituo hivyo ni pamoja na mapango ya Amboni Tanga, Kimondo cha Mbozi Songwe, Magofu ya Engaruka yaliyopo Monduli, Eneo la bonde la Olduvai na Eneo la Laetoli inayohifadhi nyazo za binadamu wa kale pamoja na miamba ya Mumba iliyoko eneo la Eyasi Wilaya ya Karatu.
0 Comments