Header Ads Widget

Responsive Advertisement

TAMASHA LA ZIFF TOLEO LA 27 RASMI KUANZA AGOSTI 1-4 2024

 



Viongozi mbalimbali walioshiriki katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF) wakionesha Bango rasmi la Tamasha la 27.



TAMASHA la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF) toleo la 27  kwa mwaka huu linatarajiwa kufanyika Zanzibar kuanzia Agosti 01 hadi 04, 2024.

Hayo yamebainishwa leo Julai 16, 2024 na Afisa Mtendaji Mkuu wa Tamasha hilo Joseph Mwale akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

"Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar ni tukio la kila mwaka lenye hadhi kubwa kwenye tasnia ya filamu. Kupitia filamu kutoka sehemu mbalimbali tamasha limekuza mabadilisho ya tamaduni na kusheherekea maboresho ya sanaa ya kutengeneza filamu," amesema Mwale na kuongeza,

"Tamasha lilianzishwa mwaka 1997 limekua jukwaa kubwa la kuwaunganisha wadau wa filamu duniani kupitia filamu. Mwaka huu  Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar linatarajiwa kufanyika Zanzibar kuanzia tarehe 01 hadi 04 Agosti, 2024,". 

Mwale amebainisha kuwa Tamasha hilo lina lengo la kuongeza uelewa wa tasnia ya filamu na kukuza sanaa hiyo barani Afrika na kwa Nchi za majahazi za  Bahari ya Hindi ikiwemo Asia ya Kusini Mashariki, Rasi ya Uarabuni, Ghuba ya Uajemi, Iran, Pakistan, India na Visiwa vya Bahari ya Hindi.

Kwamba Tamasha lina majukwaaa mbalimbali ikiwemo Jukwaa la watoto,  wanawake wa vijini, mbio ngalawa, mpira wa miguu wa wanawake ufukweni, majadiliano magumu, jukwaa la muziki na sanaa pamoja na majukwaa ya wazi ya uonyeshaji wa filamu.

Mwale ameeleza kuwa Tamasha linatarajia kua na watazamaji  zaidi ya 200,000 na kuongeza uelewa wa tasnia ya filamu huku akebainisha kwamba kauli mbiu ya mwaka huu ni Kuhuisha. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tamasha hilo Hatibu Madudu amesema Jumla ya filamu 3,000 kutoka sehemu mbalimbali za dunia zimepokelewa ambapo kutoka Afrika Mashariki  jumla ya filamu 354 zimepokelewa.

"Kenya imewasilisha filamu (16), Uganda filamu (123) wakati Tanzania filamu (62), Rwanda (12), Burundi (3).  Afrika Kusini (71). Kuna idadi kubwa ya uwasilishaji wa filamu kutoka Iran, India, Brazil, Marekani, China, Ufaransa, Misri, Italia, Uturuki, Nigeria, Argentina, Hispania, Poland, Uingereza, Ujerumani, Kanada, Indonesia, Shirikisho la Urusi, Ukraine, Jamhuri ya Korea, Falme za Kiarabu, Pakistan, Tunisia, Ugiriki, Morocco, Ghana, Senegal, Sudan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na Ethiopia, Somalia na Denmark (kutaja chache kati ya zaidi ya nchi 100+)," amebainisha Mwale na kusema.

"Kamati ya uteuzi wa filamu walikesha kuchagua filamu zenye vigezo  vinavyoakisi kauli mbiu ya mwaka huu Kuhuishwa na jumla ya filamu 60 zimechaguliwa. Filamu zilizochaguliwa ni pamoja na filamu za urefu (17),  hali halisi (13),  filamu fupi na katuni (30). Shukrani za kipekee ziwafikie wateuzi wa filamu hizo,".

Hata hivyo kwa masikitiko makubwa  ametangaza kuwa  mashindano ya Filamu za   Sembene Ousmane ambayo hapo awali yaliungwa mkono na Deutsche Gesellschaft für Internationale Entwicklung (GIZ) kwa zaidi ya muongo mmoja tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009 hayatofanyika mwaka huu kutokana na kujiondoa ghafla kwa mfadhili katika hatua za mwisho.

Ameweka wazi kuwa tuzo hii ya kifahari imekuwa chachu ya  kukuza utamaduni bora, ubunifu na uvumbuzi ndani ya jamii ya filamu ya Afrika na kwamba kusitishwa  ghafla imewakosesha  nafasi ya kurejelea kama tamasha linavyopangwa kufanyika kuanzia tarehe 1 hadi 4 Agosti, 2024.

Hivyo amesema usimamizi wa tamasha umepeleka ombi kwa GIZ kuwaomba wafikirie tena uamuzi wao angalau kwa mwaka huu huku wakiendelea kutafuta msaada kutoka kwa wafadhili wengine wenye uwezo wa kuchukua udhamini wa Mashindano ya Tuzo za Filamu za Maendeleo ya Sembene Ousmane.

Amesema mwaka huu, aina za mashindano ya filamu  ni Filamu Bora ya Urefu, Filamu Bora ya Hali Halisi, Tuzo ya Emerson kwa Filamu Bora ya Zanzibar, Filamu Fupi Bora au Katuni Bora, Filamu Bora ya Afrika Mashariki, Mwigizaji Bora (Afrika Mashariki), Mwigizaji Bora wa Kike (Afrika Mashariki), Mwigizaji Bora (Tanzania) na Mwigizaji Bora wa Kike (Tanzania).

Ningine ni tuzo ya Mwenyekiti wa ZIFF na Tuzo ya Mafanikio ya Maisha pamoja na Tuzo ya Chaguo la Watu ambayo inahifadhiwa kwa Mfululizo wa Drama za Televisheni kutoka Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) (Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Somalia na Jamhuri ya Kongo). 

Amesema kura za umma zimepangwa kuanza Julai 20 hadi Agozti 03, 2024 na katika mkutano huo na waandishi wa habari wametumia fursa hiyo kuzindua Bango la Tamasha la 27. 

Post a Comment

0 Comments