SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeagiza kufungwa Kanisa la Christian Life Church linaloongozwa na Mchungaji Domique Kashoix Dibwe maarufu Kiboko ya Wachawi, lililopo Buza Kwa Lulenge, Temeke - Dar es Salaam baada ya kanisa hilo kwenda kinyume cha taratibu za usajili.
Barua ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya za Kiraia ya Julai 25, 2024 imewaelekeza Mwenyekiti wa Kanisa la Christian Life Church na Mchungaji Dominique Kashoix Dibwe kufunga tawi la Kanisa hilo linaloendeshwa na mchungaji huyo.
Miongoni mwa sababu zilizotajwa za kufungwa kwake ni kutoa mafundisho yenye kuleta taharuki katika jamii na mahubiri ambayo ni kinyume na maadili, mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania.
Madai mengine ni kutoa mahubiri yanayodhalilisha watu madhabahuni, kutoa mahubiri chonganishi na kuhamasisha waumini wa kanisa lake kuua watu kwa dhana au tuhuma za uchawi au ushirikina.
Baada ya kusambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kwamba Serikali imeagiza kufungwa Kanisa hilo, baadhi ya vitu kanisani hapo vimeondolewa.
0 Comments